![]() |
MAJERUHI WA AJALI |
“Majeraha makubwa na damu iliyokuwa ikichuruzika
kutoka katika miili ya watu ilifanya nifikiche macho yangu kila mara ili
kujiaminisha kile ninachokiona mbele yangu.”
Anasema hakutegemea safari yake ya kwenda Mwanza ingefupishwa ghafla namna ile.
Katika ajali hiyo iliyotokea Septemba mwaka huu,
zaidi ya watu 37 walifariki dunia na wengine 78 kujeruhiwa vibaya. Ajali
hiyo ilihusisha mabasi ya Mwanza Coach na J4 Express.
Asha anaeleza kuwa anakumbuka siku ya tukio
alikuwa amepanda Mwanza Coach lililokuwa likielekea mkoani Mwanza.
Alikuwa akienda kwenye shughuli zake. Anasema baada ya basi kwenda kwa
muda wa nusu saa tu, lilitokea tukio la kutisha ambalo linamfanya
aendelee kuhisi labda yupo ndotoni.
Anasema anakumbuka alikuwa kwenye kiti cha pili
kutoka mwisho, kwa hiyo ilikuwa ni vigumu kuona kilichokuwa kikitokea
mbele yao na badala yake alishtukia kishindo kikubwa na baadaye viti vya
mbele kung’ooka na kuwaponda waliokuwa wamekaa nyuma.
Asha anasimulia kuwa alishuhudia watu wakiwa na
majeraha ya ajabu wakiwa wametapaa damu kila mahali huku wengi wao
wakilia kwa uchungu na wengine wakionekana kukata roho.
“Kwa kweli ajali ilikuwa ni mbaya,” anasema.
“Nilimshuhudia baba mmoja akiwa amekatika shingo na kichwa kutenganishwa
na kiwiliwili… niliogopa sana na kushikwa na butwaa, nikawa kama vile
sielewi kinachoendelea.”
Anasema kuwa baadaye aliungana na abiria wengine
waliokuwa wakilia kuomba msaada baada ya yeye na wengine watatu
kuokolewa na watu wasiowafahamu kwa kupitishwa madirisha ya nyuma.
Binti huyo anasema hajui alinusurika vipi katika
ajali hiyo kwani abiria wenzake wengi aliokaa nao viti vya nyuma nao
walipoteza maisha.
Naye majeruhi mwingine, Frank Samson (35) mkazi wa
Mwanza ni miongoni mwa walionusurika katika ajali hiyo mbaya ambaye
anaeleza namna alivyoshuhudia ajali hiyo.
Frank, ambaye siku ya tukio alikuwa akisafiri na
basi la Mwanza Coach akitokea Musoma kwenda Mwanza, anasema kuwa siku
hiyo walianza safari saa 4:30 asubuhi wakitokea kituo kikuu cha mabasi
iliyopo eneo la Bweri mjini Musoma.
Anasema kuwa dakika chache baada ya kufika Kitongoji cha Irimba
Kijiji cha Sabasaba, ghafla gari dogo aina ya Land Cruiser lenye rangi
nyeusi lilipita basi lao, likiwa katika mwendokasi bila kuchukua
tahadhari ya aina yoyote.
Anasema kwa mujibu wa sheria za usalama
barabarani, gari hilo dogo lilipaswa kusubiri kwanza kabla ya kuchukua
uamuzi wa kulipita basi kwa vile eneo hilo ni lenye mteremko mkali na
kuna daraja, lakini dereva wa gari hilo hakuzingatia hilo.
Anaeleza kuwa wakati gari hilo likiwa katika
harakati za kulivuka basi lao, ghafla walikutana na basi jingine la J4
lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Sirari wilayani Tarime.
Kama ilivyokuwa kwa upande wao, kufumba na kufumbua gari dogo liligongwa na mabasi yote mawili kwa ubavuni na kurushwa mtoni.
Anasema baada ya gari hilo kugongwa, mabasi hayo
mawili yaligongana uso kwa uso na kusababisha vifo vingi na majeruhi
wengi. Anasema ajali hiyo ilitokana na mwendo wa mabasi hayo hasa
ikizingatiwa kuwa yote yalikuwa kwenye mteremko mkali.
Frank anafafanua kuwa, baada ya ajali hiyo
hakumbuki kilichoendelea kwani alipoteza fahamu na kujikuta akiwa
amezungukwa na watu huku akiwa amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Akiongea kwa uchungu, anasema kuwa katika ajali
hiyo wafanyakazi wenzake wote wa basi hilo, ambao ni dereva na utingo,
walipoteza maisha papo hapo.
“Inaniuma sana wafanyakazi wenzangu tuliokuwa nao
katika basi kupoteza maisha. Sijui ilikuwaje nikanusurika, kikubwa
namshukuru sana Mungu,” anafafanua kwa huzuni.
Anasema kuwa kupona kwake ni muujiza wa Mungu
kwani tukio hilo lilikuwa kubwa hasa ukizingatia idadi ya watu
waliopoteza maisha katika ajali hiyo na kuongeza kuwa hana cha kumlipa
Mungu zaidi ya kusema ahsante.
Ajali ya kihistoria
Ajali hiyo inasemekana imevunja rekodi ya ajali zilizowahi kutokea mkoani Mara kwa kipindi cha zaidi ya miaka 19.
Ajali kubwa kuwahi kutokea ilihusisha basi la
Busigasore lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Musoma. Basi hilo
lilipoteza mwelekeo wakati likijaribu kukwepa gari dogo aina ya Land
Rover 109 katika eneo la Kiabakari wilayani Butiama mwaka 1995.
Katika ajali hiyo jumla ya watu 35 walipoteza maisha huku idadi kubwa ya watu wakijeruhiwa.
Vifo vya ajali
Jumla ya watu 1,126 wamepoteza maisha kwa ajali za
barabarani katika kipindi cha miezi mitatu huku kukiwa na majeruhi
3,827 kati ya ajali 3338 zilizotokea katika maeneo tofauti nchini.
Takwimu hizo zilitolewa wiki iliyopita na Waziri
wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe alipokuwa akifungua mkutano wa
mazungumzo ya pamoja na wamiliki wa mabasi ya kusafirisha abiria.
Dk Mwakyembe alisema katika ajali hizo, zaidi ya
asilimia 90 zilitokana na uzembe wa madereva ambao wengi wamekuwa
hawajali sheria za barabarani ikiwamo kuendesha vyombo hivyo wakiwa
wamelewa.
Waziri alitaja ajali hizo kwamba zilitokea katika
kipindi cha Juni Mosi hadi Septemba 8 na kwamba kila mwezi kulikuwa na
ongezeko la vifo.
“Juni tulipata ajali 1,157, zikasababisha vifo vya
watu 320 na majeruhi 1,189, Julai zilikuwa ajali 1,035, vifo vikawa 368
na majeruhi 1,261 wakati Agosti ajali zilikuwa 1,146 kukawa na vifo 390
na majeruhi 1,365,” alisema Mwakyembe.
Waziri alisema kipindi hiki siyo cha kulaumiana na badala yake kila mmoja atimize wajibu kwa kuwa Watanzania wanaangamia.
Kiongozi huyo aliwataka wamiliki kutulia na
kufanya uchambuzi wa kina juu ya nini kinasababisha ajali kuongezeka
mwezi hadi mwezi na kuwa karibu na madereva na watumishi wengine kwenye
mabasi.
Akizungumza katika Mkutano huo, Katibu wa Chama
cha Wenye Mabasi (Taboa) Enea Mrutu alikiri ajali nyingi kusababishwa na
uzembe wa madereva ingawa yeye alisema ni kwa asilimia 70.
Hata hivyo, Mrutu alisema bado kuna kazi katika
vyombo vya usimamizi ikiwamo polisi ambao wamekuwa wakiwanyanyasa
madereva na kuwachelewesha jambo linalofanya kuongeza mwendo
wanapoachiwa.
Kingine Katibu huyo alilalamikia ni vyuo vya
usafiri ambavyo hutoa madereva ambao mwishowe wanaonekana kutokukidhi
viwango wakati vyuo hivyo vipo chini ya Serikali.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment