Mbunge wa Bariadi Magharibi (UDP) na Mjumbe wa Bunge la Katiba, John Cheyo.
Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, John Cheyo juzi aliomba
mwongozo wa mwenyekiti akidai kuwa taarifa iliyosomwa bungeni na
Mwenyekiti wa Kamati namba 11, Anne Kilango ni tofauti na ile
waliyoijadili.
Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi
(UDP), alisema: “Pamoja na heshima zote za mheshimiwa aliyeisoma
(taarifa), lakini mimi nilikuwa mmojawapo wa wajumbe wa kamati ya 11.
Mengi ambayo aliyosoma hatukuyazungumza,” alisema Cheyo na kuongeza:
“Sasa hii inatupa taabu tunafanyaje sasa? Maana
yake sisi tumerekebisha mambo mengi, ya uraia tumesema pawapo na fursa
ya uraia wa nchi nyingine, yote hayakusemwa.”
Cheyo alisema mambo muhimu hayakusemwa labda ni
kwa sababu wajumbe wa kamati hiyo hawakupata fursa ya kuitwa na
kuipitisha taarifa hiyo.
“Tungepata nafasi ya kuipitisha tungesema hili hapana, hili sawa,” alisisitiza Cheyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta
alisema tatizo huenda likawa ni muda, kwani mambo mengi yapo kwenye
kitabu lakini kutokana na muda hayakusomwa.
“Tatizo ni muda tu, ukisoma hayo ya uraia kwenye
kitabu hiki yapo tu. Mimi nadhani uwasilishaji tu kwa sababu tunakatiza,
tunagonga kengele hapa, lakini ukitazama kwenye ukurasa wa 25 mpaka 26
mpaka 27 yapo,” alisema.
Jana, Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hamad
alisema tatizo lilitokana na kamati ya Kilango kutofanya uhakiki wa
maandishi na kuwa wameelezwa wahakikishe wanahakiki kazi yao kabla
haijapelekwa kusomwa bungeni.
No comments:
Post a Comment