Dar es Salaam. Pazia la Ligi Kuu Bara limefunguliwa rasmi jana, lakini ni timu tatu zinapewa nafasi kubwa ya kuwa mabingwa wa ligi hiyo msimu ujao, ambazo ni bingwa mtetezi Azam FC, Yanga na Simba.
Licha ya timu zote hizo kuwa na nafasi kubwa ya
kutwaa ubingwa, Yanga imeonekana kuwa imara zaidi katika eneo la
ulinzi, wakati Azam ikiwa balaa katika kuzifumania nyavu kuliko wenzake,
huku Simba ikiwa haieleweki.
Safu ya ulinzi ya Yanga inaonekana kutopitika
kirahisi na hivyo washambuliaji wa timu pinzani kwenye ligi wanatakiwa
kuwa na akili za ziada kuipenya ngome hiyo inayoongozwa na Kipa
Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub
‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani.
Ngome ya Yanga haijaruhusu bao katika mechi tano
ilizocheza chini ya kocha mpya, Marcio Maximo, mechi nne zikiwa za
kirafiki na moja ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.
Mabingwa hao wa zamani wana washambuliaji, wanane
ambao ni Genlison Santos ‘Jaja’, Andrey Coutinho, Mrisho Ngassa, Simon
Msuva, Jerry Tegete, Said Bahanuzi, Hussein Javu na Hamis Kiiza.
Azam yenyewe imeonekana kuwa hatari zaidi upande
wa kuzifumania nyavu kwani katika mechi 12 ilizocheza zikiwamo za
kirafiki, michuano ya Kagame na Ngao ya Jamii, imefunga mabao 20.
Safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inaongozwa na Kipre Tchetche, John Bocco, Leonel Saint-Preux, Didier Kavumbagu.
Licha ya Azam kuonekana iko kamili kwa
kuzifumania nyavu, ukuta wake imeonekana kulegalega kwani katika michezo
12, safu ya ulinzi imeruhusu mabao 11.
Safu ya ulinzi inaongozwa na Mwadini Ally, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni , David Mwantika/Said Morad na Aggrey Morris.
Timu nyingine inayopewa nafasi ya kutisha ni Simba
ingawa imeonekana haisomeki kwani bado inayumba katika safu yake ya
ulinzi baada ya kumuondoa Donald Mosoti, hivyo kubaki na beki mzoefu,
Joseph Owino ambaye atasaidia na chipukizi Hassan Isihaka na Joram
Mgeveke.
Simba imeonekana kuwa na safu bora ya ushambuliaji
katika mechi sita za kirafiki ilizocheza, imefunga mabao 12 na
imefungwa matatu, safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Ammis Tambwe,
Emmanuel Okwi, Elius Maguri, Paul Kiongera, Ramadhan Singano na Haruna
Chanongo.
No comments:
Post a Comment