
Kiongozi mwandamizi wa kundi la
wanamgambo wa Al Qaeda anayeshukiwa kupanga kulipuwa treni mijini New
York na London ameuawa nchini Pakistan,kwa mujibu wa Jeshi la nchi hiyo.
Adnan
el Shukrijumah aliuawa katika shambulizi kazkazini magharibi mwa
Pakistan karibu na mpaka wa Afghanistan,jeshi hilo limesema.
Maafisa
wa kundi la Ujasusi kutoka Marekani FBI wamekuwa wakimtaja kuwa mkuu wa
kitengo cha oparesheni katika kundi la Al Qaeda,wadhfa ambao
ulishikiliwa na mtu anayeshukiwa kupanga njama za shambulizi la Septemba
11 Khalid Sheikh Mohammed.
Shukrijumah alizaliwa nchini Saudi Arabia na kuishi kwa miaka kadhaa nchini Marekani.
Aliorodheshwa
katika mashtaka kama muhusika wa kupanga njama katika kesi dhidi ya
watu watatu wanaoshutumiwa kwa kupanga mashambulizi ya kujitolea muhanga
katika barabara za treni mjini New York mwaka 2009.
Pia anashukiwa kupanga njama za kutekeleza mashambulizi ya kundi ya Al Qaeda nchini Panama,Norway na Uingereza.
Uvamizi
huo wa mapema leo ulifanyika katika jimbo la Shinwarsak kusini mwa
Waziristan,ambalo ni eneo la Kazkazini magharibi mwa mkoa uliopo karibu
na mpaka.
Jimbo hilo ni kambi ya wapiganaji wa Taliban nchini Pakistan na washirika wao.
No comments:
Post a Comment