Polisi wa Beijing, China hatimaye wamemkamata rasmi mtoto wa mkali wa
Martial Arts Jackie Chan anaefahamika kwa jina la Jaycee Chan kufuatia
tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.
Taarifa kutoka katika ofisi ya mwendesha mashitaka wa wilaya ya
Dongcheng, zimethibitisha hatua hiyo ambapo Jaycee Chan anaweza kufungwa
hadi miaka 3 jela endapo atakutwa na hatia ya kuwaruhusu watu kutumia
dawa za kulevya katika nyumba yake.
Jaycee Chan alikamatwa mwezi uliopita akiwa na muigizaji mwingine wa
Taiwan anaefahamika kwa jina la Ko Kai. Wawili hao walifanyiwa vipimo na
kugundulika kuwa walitumia dawa za kulevya aina ya Marijuana na
walikiri kuwa walipeleka nyumbani kwa Jaycee grams 100 za dawa hizo.
Kwa sheria za China, Polisi anatakiwa kuomba ruhusa ya kumkamata
rasmi mtuhumiwa kutoka kwa muendesha mashitaka wa serikali. Taratibu za
upelelezi zinaweza kuendelea wakati huo.
Kwa upande wa Ko Kai, alipewa kifungo cha siku 14 baada ya kukiri
kutumia marijuana na baadae yeye na familia yake walifanya mkutano na
waandishi wa habari na kuomba radhi kwa kitendo hicho.
No comments:
Post a Comment